Marekani imewatahadharisha raia wake wanaoitembelea Kenya kuwa kuna taarifa za kiintelijensia zinazoonesha kuwa magaidi wanaweza kushambulia maeneo ya Kenya wakiwalenga wageni kutoka Magharibi.
Onyo hilo la Marekani limekuja ikiwa ni wiki kadhaa tu tangu kundi la kigaidi la Al-Shabaab litekeleze shambulizi lililosababisha vifo vya watu 21.
Raia wa Marekani na Uingereza ni moja kati ya waliopoteza maisha kwenye tukio hilo lililodumu kwa takribani saa 19.
Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi nchini Kenya umeeleza kuwa mashambulizi yanaweza kulenga maeneo ya Nairobi, Naivasha, Nanyuki na fukwe maarufu zenye raia wa kigeni.
“Ubalozi wa Marekani unawakumbusha raia wa Marekani kuendelea kuwa makini wanapokuwa nchini Kenya, hususan kwenye maeneo ya wazi kama maduka makubwa, hoteli na sehemu za kuabudia,” imeeleza taarifa hiyo.
Kadhalika, Ubalozi wa Uingereza nchini Kenya, umetuma ujumbe kwenye mtandao wao kuwashauri wageni sehemu za kutembelea ukieleza kuwa, “magaidi wanaweza kufanya majaribio ya shambulizi nchini Kenya.”
Serikali ya Kenya imeahidi kupambana na magaidi wanaolenga kudidimiza uchumi wa nchi hiyo katika sekta ya utalii na kuchukua uhai wa watu wasio na hatia.
Jeshi la Kenya limeendelea kushirikiana na vikosi vya Umoja wa Mataifa kupambana na Al-Shabaab nchini Somalia.