Tukiwa tunakamilisha mwaka 2018 tukisubiri neema ya kuuona mwaka 2019, tujikumbushe tukio la aina yake lililofanyika usiku wa Novemba 30 mwaka huu.
Kwa mara ya kwanza, mashindano ya kumtafuta mrimbwende na mtanashati mwenye ulemavu wa ngozi (albino) katika Ukanda wa Afrika Mashariki yamefanyika jijini Nairobi nchini Kenya.
Jumla ya vijana 30 walishiriki katika mashindano hayo kutoka nchi za Kenya, Uganda na Tanzania, ambapo Mtanzania Silas Shedrack mwenye umri wa miaka 20 pamoja na Mkenya Maryanne Muigai mwenye umri wa miaka 19 walishinda mataji kama ‘Mr na Miss Albinism East Africa’.
Washindi wa shindano hilo walizawadiwa fedha pamoja na mikataba ya mwaka mmoja kufanya kazi kama mabalozi wa makampuni ambayo ni wadau wa kuunga mkono haki za albino katika ukanda huo.
Shindano hilo lililopewa jina la ‘Beauty Beyond the Skin’, halikuwa shindano la urembo pekee bali lililenga katika kuhamasisha kupiga vita unyanyapaa na mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi barani Afrika.
Taasisi ya Umoja wa Albino nchini Kenya (Albinism Society of Kenya) kwa kushirikiana na taasisi nyingine kutoka Tanzania na Uganda ilifanikisha kufana kwa mashindano hayo.
Washiriki walikaa kambini kwa kipindi cha siku 10 kwa ajili ya kupata mafunzo ya kushiriki mashindano hayo pamoja na mambo ya kijamii na kujiamini.
“Shindano hili limenisaidia kuongeza uwezo wa kujiamini na kujikubali. Kuweza kusimama mbele ya umati wa watu kwenye tukio letu ni uzoefu mkubwa. Nimefurahi sana,” Aljazeera inamkariri Sherleen Tunai Lumumba ambaye ni mshiriki kutoka Kenya.
“Nimekutana na watu wengi na kupata marafiki wengi kutoka sehemu mbalimbali barani Afrika kutokana na tukio hili,” aliongeza.
Watu wenye ulemavu wa ngozi (albino) wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na tishio la kuuawa kutokana na imani za kishirikina katika nchi nyingi za Afrika.