Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema kuna mashirika yanatakiwa yafuatiliwe, kwani hayatakiwi kuwepo kutokana na kuendelea kula fedha za Wananchi bila kuzalisha, akitolea mfano wa NDC.
Rais Samia ameyasema hayo wakati wa kupokea ripoti za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa – TAKUKURU hii leo Machi 29, 2023 Ikulu jijini Dar es Salaam.
Amesema, “kufikia hapa tulipo kuna mashirika hayatakiwi kuwepo au yalishapitwa na wakati mengine hayajawahi kufanya kazi ikawa na ‘positive impact’ (matokeo chanya), mfano NDC toka nipo Sekondari nalisikia kwa wale wa umri wangu.”
Rais Samia ameongeza kuwa, “tangu nipo Sekondari mpaka leo nakalia kiti hiki NDC wapo lakini ukitafuta wanafanya nini ambacho kimeleta matokeo gani utakuta labda ile awamu ya kwanza kule walipoundwa lakini si katika awamu ya pili, si ya tatu, si ya nne, si ya tano si hii, lakini bado dude NDC lipo.”
Hata hivyo amebainisha kuwa, “haya mashirika yanakula tu pesa Serikalini lakini yenyewe hayaleti nendeni kayaangalieni mashirika ya namna hii yapo mengi, madhumuni ya kuundwa kwake ni yaende yakazalishe halafu yalete pesa Serikalini lakini hayaleti, nendeni mkafuatilie.”