Mashirika ya kimataifa kutetea haki za binaadamu, Amnesty International na International Commission of Jurists, wametoa ripoti inayotaka uchunguzi wa vizuizi vya Taliban dhidi ya haki za wanawake na wasichana Afghanistan
Ripoti hiyo iliyopewa jina Vita vya Taliban kwa wanawake: Uhalifu dhidi ya ubinaadamu wa unyanyasaji wa kijinsia nchini Afghanistan, iliinukuu sheria ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC inayoorodhesha unyanyasaji wa kijinsia kama uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Aidha, Ripoti hiyo imelezea juu ya vikwazo vikali vilivyowekwa na Taliban kwa wanawake na wasichana, baada ya kurejea mamlakani Agosti 2021 wakati wanajeshi wa Marekani na NATO kuondoka nchini humo baada ya miongo miwili ya vita.
Katika hatua nyingine, ripoti hiyo imelishutumu kundi la Taliban kwa kuwalenga wanawake na wasichana walioandamana kwa amani kwa kuwaweka kizuizini, kuwatowesha kwa nguvu na kuwaweka chini ya ulinzi.