Wakili wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mwendesha Mashtaka ya Serikali Mkoani Tanga, Lucky Titus Kaguo amesema kesi zinazopokelewa kwa wingi mkoani humo ni za biashara ya dawa za kulevya, ukatili wa kijinsia, ulawiti na ubakaji.
Wakili Kaguo ameyasema hayo, wakati akizungumza na wanafunzi wa shule za Sekondari na Msingi za Jijini Tanga, waliotembelea Banda lililopo viwanja vya Urithi Jijini humo yanapoendelea maonyesho ya wiki ya Sheria Tanzania kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa huku akieleza mkakati ambao wameupanga kuweza kukabiliana na vitendo hivyo.
Amesema, mkakati wa kwanza ni kwamba wanakusudia kuandaa mpango wa kutoa elimu kwa wananchi na wanafunzi juu ya athari ya vitendo hivyo ili kuweza kuibadilisha jamii iondokana navyo na kwamba “Kwa mkoa huu tunapata shida kwenye makosa ya jinai aina mbili madawa ya kulevya na unyanyasaji wa kijinsia ubakaji na ulawiti makosa ambayo yameshamiri sana kwa mkoa wa Tanga“.
Aidha, amesema kutokana na uwepo wa hali hiyo wanaandaa mpango wa kuzunguka kwenye shule za msingi na sekondari ikiwemo kukutana na wanafunzi, wananchi na kuwaeleza umuhimu wa kutoa taarifa za unyanyasaji unapotokea.
Hata hivyo, alisema kwamba wameshiriki kwenye maonyesho hayo ya wiki ya sheria kutoa elimu kwa wanafunzi na wananchi kwa kutatua matatizo yao na kuwaleta wananchi kuhusu ofisi hizo na kueleza majukumu yao na kutatua matatizo yao.
Kaguo amewaeleza umuhimu wa ofisi hizo katika mashauri wanayopalekwa na wananchi huku wakieleza jitihada za serikali katika kutatua mashauri yake kwa nia ya usuluhihi badala ya njia ya mahakama.