Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar – ZAFELA, na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar – TAMWA ZNZ, wamelipongeza Jeshi la Polisi kwa kuharakisha uchunguzi na kupatikana kwa mtuhumiwa wa kesi ya mauaji ya Khairat Juma Bakari, ambae aliuawa Mei, 2023.
Hatua hiyo, inafuatia bada ya Jeshi la Polisi Zanzibar kutoa taarifa ya kukamatwa kwa mtuhumiwa Yusuf Ame Abubakar, ambaye anatuhumiwa kwa mauaji ya Khairat yaliyotokea eneo la Mbuzini Wilaya ya Magharibi “A” Unguja na kuripotiwa na vyombo vya habari Mei 20, 2023.
ZAFELA na TAMWA-ZNZ wamelishukuru Jeshi la Polisi kwa hatua hiyo muhimu na kuliomba kuharakisha pia uchunguzi wa mauaji ya Laura Msemwa, yaliyotokea katika kipindi kama hicho, ili mtuhumiwa aweze kupatikana na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Aidha, jumuiya hizo pia zimetoa wito kwa jamii kuendelea kutoa mashirikiano kwa Jeshi la Polisi katika kuwasaka wahalifu mbalimbali wa makosa ya jinai, ili waweze kukamatwa na hatimae kupunguza ama kumaliza matukio ya kihalifu visiwani Zanzibar.
Khairat Juma Bakari na Laura Msemwa waliripotiwa kuuawa kikatili katika mazingira ya utata huku Wanaharakati wa haki za binadamu wakiyatafsiri mauaji hayo kama mwendelezo wa mashambulizi dhidi ya wanawake yanayokithiri na uwepo wa ukatili wa kijinsia visiwani humo.
Awali, kupitia taarifa ya pamoja ya Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake – TAMWA, – Zanzibar na Jumuia ya Wanaseheria Wanawake Zanzibar – ZAFELA, ya Mei 28, 2023, walilitaka Jeshi la Polisi kuwatia nguvuni watu waliohusika na matukio hayo ya kihalifu.