Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Walemavu, Anthony Mavunde ameutaka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kuiburuza mahakamani Shule ya Scolastica na Kampuni ya Usafirishaji ya Machare Investment kutokana na kutojisajili na mfumo huo.
Ametoa agizo hilo katika ziara yake ya kushtukiza na kuwabaini waajiri ambao bado hawajatekeleza takwa la kisheria linalowataka kujisajili katika mfuko huo.
Amesema kuwa sheria ya mfuko huo kifungu cha 71(4) cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi inasema endapo mwajiri akipatikana na hatia adhabu yake ni kulipa faini isiyozidi Sh50 milioni au kifungo cha miaka mitano jela au vyote kwa pamoja na kwamba Serikali haitamuonea huruma mwajiri ambaye hatafuata sheria hiyo badala yake itamburuta mahakamani.
“Serikali imeshatoa matamko mbalimbali yanayowahimiza waajiri kutekeleza takwa hilo la kisheria na leo hii hakuna njia nyingine, waajiri hawa tuliowabaini hapa mkoani Kilimanjaro naagiza WCF iwapeleke mahakamani haraka iwezekanavyo ili sheria ichukue mkondo wake,”amesema Mavunde
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa mfuko huo, Anslem Peter amesema kuwa waajiri 1,039 na kwamba 525 ndio wamejisajili huku 514 wakiwa hawajajisajiliwa.