Baraza la Kisekta la Mawaziri wa Biashara, Viwanda, Fedha na Uwekezaji (SCTIFI) la Jumuiya ya Afrika Mashariki lakubaliana kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara na kuimarisha biashara na uwekezaji ndani ya Jumuiya hiyo.
Awali akifungua mkutano Jijini Arusha Ijumaa, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote amesema kuwa mkutano huo ni muhimu kwani utawawezesha mawaziri kupitia na kujadili miongozo ambayo itasaidia kuboresha biashara katika ukanda wa Afrika Mashariki ikiwemo kuondoa vikwazo visivyo vya kibiashara.
Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, na Mkuu wa Ujumbe wa Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo amesema kuwa mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wamekubaliana mambo mengi ya msingi ikiwemo kuendelea kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kikodi.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Geofrey Mwambe amesema kuwa mawaziri wamekubaliana kutoa msukumo wa biashara katika jumuiya ya Afrika Mashariki lizingatiwe na kupea kipaombele na kuruhusu sekta binafsi kufanya biashara katika nchi mbalimbali.
Mkutano huo umehudhuriwa na Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Kenya, Betty Maina, Waziri wa Viwanda na Biashara, – Tanzania, Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Geofrey Mwambe, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda – Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban.
Wengine ni Waziri wa Biashara na Viwanda wa Rwanda, Mhe. Beata Habyarimana, Waziri wa Biashara, Viwanda na Ushirika wa Uganda, Mhe. Grace Choda, pamoja na Katibu Mkuu, Wizara ya Biashara, Uchukuzi, Viwanda na Utalii wa Burundi, Balozi Jeremie Banigwaninzigo.
Mkutano huu ni maelekezo ya Wakuu wa Nchi na Serikali katika ziara ya Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyoifanya nchini Kenya tarehe 04 hadi 05 Mei, 2021.