Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele ameshusha Presha za Mashabiki wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Young Africans, ambao walikua wakiyumbishwa na taarifa za kuondoka kwake katika kipindi hiki cha usajili.
Mayele alihusishwa na mpango wa kuwaniwa na Klabu ya Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, Raja Casablanca ya Morocco na Al Hilal ya Sudan, huku ikidaiwa klabu hizo zilitenga dau nono ambalo lingemng’oa Young Africans.
Baada ya kuwasili nchini mwanzoni mwa juma hili akitokea kwao DR Congo, Mshambuliaji huyo alianza mazoezi na wenzake Kambini Kigamboni, huku akionekana kuwa na furaha muda wote.
Jana Jumatano (Julai 27), Azam TV ilifanya mahojiano na Mayele ili kufahamu mustakabali wake ndani ya Young Africans, huku viongozi wa juu wakidai hataondoka kutokana na mkataba uliopo baina ya pande hizo mbili.
Mayele alisema bado ataendelea kuwa sehemu ya kikosi cha Young Africans kwa msimu ujao, kwani bado ana mkataba wa mwaka mmoja, baada ya kuitumikia klabu hiyo msimu uliopita.
Amesema Mashabiki wanapaswa kuendelea kuamini hilo, na amewaahidi kufanya makubwa zaidi ya ilivyokua msimu uliopita, ambapo alimaliza nafasi ya pili katika orodha ya ufungaji bora, akitanguliwa na Mshambuliaji mzawa George Mpole.
“Kwanza ninamshukuru Mungu kwa kurudi salama, tumeshaanza maandalizi ya msimu ujao hapa kambini kwetu Avic Town, nafahamu ni kipindi kigumu, lakini sina shaka na hilo kwa sababu natarajia makubwa sana na timu yangu.”
“Ni kweli Kaizer Chiefs na Klabu nyingine za Afrika zilihitaji nijiunge nazo katika kipindi hiki, lakini hawa wa Afrika Kusini, Raja Casablanca ya Morocco na Al Hilal ya Sudani ndio walikua na ofa kubwa zaidi,”
“Mimi bado ni mchezaji wa Young Africans bado nina mkataba wa miaka miwili, nimeshamaliza mwaka wangu mmoja. Nataka kuongea ukweli kabisa hapa, sijaja Young Africans kwa mkopo, hapa nina mkataba halali kabisa.” amesema Mayele