Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele amesema kila mchezo ni muhimu kwao lakini kwa upande wa kimataifa ni muhimu zaidi kwa sasa kwa sababu imebaki michezo miwili ambayo inatakiwa kuwaweka kwenye levo nyingine.
Young Africans itacheza dhidi ya US Monastir ya Tunisia siku ya Jumapili (Machi 19) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku ikihitaji alama tatu, ambazo zitawavusha hadi Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Mayele ambaye tayari ameshafunga mabao mawili katika Hatua ya makundi, amesema wanachokifanya kwa sasa ni kujiandaa kikamilifu, ili kufanikisha lengo la kupata ushindi katika Uwanja wa nyumbani.
Amesema ni kweli wanakabiliwa na Michuano ya Ligi Kuu ambayo wapo katika nafasi nzuri ya kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’, lakini kwa sasa wamegeuzia nguvu zao kwenye mchezo wa Kimataifa ambao wanapaswa kushinda.
“Ukitazama kwenye ligi kuna mechi nyingi kidogo ambazo tukipambana zaidi tutakuwa mabingwa. Ila huku kwenye shirikisho tuna mechi mbili ambazo zitaamua hatma yetu.”
“Naiwaza zaidi timu yangu kwa sasa ili iweze kufanikiwa kwenye kila hatua na kisha nawaza mimi pia malengo yao niliyojiwekea, kwenda robo fainali shirikisho ni mipango ya timu na mimi pia,” amesema Mayele
Katika msimamo wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika Young Africans ipo nafasi ya pili baada ya kucheza michezo minne, ikijikusanyia alama 07, ikitanguliwa na US Monastir ya Tunisia yenye alama 10.
TP Mazembe ya DR Congo ipo nafasi ya tatu katika msimamo wa Kundi D, ikiwa na alama 03 baada ya kucheza michezo minne hadi sasa, na AS Real Bamako ya Mali inaburuza mkia ikiwa na alama 02.