Beki kutoka nchini Ivory Coast na Klabu ya US Monastir, Ousmane Outtara amesema wameingiwa hofu kuelekea mchezo wa Mzunguuko watano wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya wenyeji wao Young Africans,.

Young Africans itaikaribisha US Monastir kutoka Tunisia katika Uwanja wa Benjamin Mkapa siku ya Jumapili (Machi 19) kwa ajili ya mchezo huo, ambao utaamua hatma ya Wananchi kutinga Hatua ya Robo Fainali kwa mara ya kwanza.

Outtara ambaye amewahi kucheza katika klabu ya AS Vita ya DR Congo sambamba na Mshambuliaji Fiston Mayele, ameeleza ugumu wa Mchezo huo pamoja na hofu ya kukamilisna na Mshambuliaji huyo.

“Ninaufahamu vyema Uwanja wa Mkapa, nimewahi kwenda pale na AS Vita, kule watu wanapenda sana mpira na ni ngumu kupata matokeo kirahisi.”

“Young Africans wamepata ushindi katika michezo miwili mfululizo hivyo naamini tunakwenda kukutana na changamoto pale, siyo rahisi kupata matokeo lakini naamini tumejiandaa vyema kupata matokeo mazuri.”

“Mayele ni mchezaji mzuri sana, ni mshambuliaji ambaye amekamilika, anafunga kila aina ya bao ambalo mshambuliaji anatakiwa kufunga.”

“Katika mchezo uliopita tulifanikiwa kucheza naye lakini haikuwa rahisi, najua tukiwa ugenini pia tutakutana na mtihani wa kukabiliana naye, lakini tutapambana naye ili asitusumbue,” amesema beki huyo

Hadi sasa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Young Africans wamecheza michezo miwili kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam dhidi ya TP Mazembe na Real Bamako ambapo michezo yote hiyo wamefanikiwa kushinda. Wakiifunga TP Mazembe 3-1 na kasha wakaiadhibu AS Real Bamako 2-0.

Mayele: tunataka kujiweka LEVO nyingine
Jeshi laingilia kati mgomo wa Madaktari, Polisi washika doria