Jeshi la Polisi Mkoani Kigoma, kwa kushirikiana na askari wa uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe wamefanikisha kukamata mtu mmoja anayeaminika kuwa mtumishi wa afya katika Halmashauri ya Wilaya Uyui mkoani Tabora, akiwa na vipande 14 vya meno ya tembo.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa mwishoni mwa mwezi uliopita katika Kijiji cha Kidyama, Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Aidha, Kamanda Makungu ambaye hakutaja jina la mtuhumiwa kutokana na sababu za kiupelelezi, amesema kuwa meno hayo yenye uzito wa kilo 20.4 yana tahamani ya shilingi 26.4 milioni.
Mkuu wa kikosi cha misitu na Uhifadhi wa Hifadhi ya Taifa ya Gombe, Yustin Njamasi amesema kukamatwa kwa vipande hivyo vya meno pamoja na mtuhumiwa kunatokana na taarifa za wananchi.