Jeshi la Polisi mkoani Mbeya, linamshikilia Mwalimu Elisha Chonya kwa tuhuma za kuwakalisha chini wanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Sinde na kisha kuwapiga picha na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii akimainisha kuwa kuna uhaba wa madawati.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo mbele ya Waandishi wa Habari na kusema mtuhumiwa alikuwa mwalimu wa mafunzo ya vitendo na sio mwajiriwa.

Amesema, “Taarifa zilisambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha wanafunzi wakiwa wamekaa chini kwenye chumba kimoja cha darasa kwa madai ya uhaba wa madawati sio za kweli ni uzushi na kuwataka wananchi kuzipuuza kutokana na kuzua taharuki.”

Mbeya – Tanzania.

Malisa ameongeza kuwa, Mwalimu  Mkuu, Anatalia Luwungo amemueleza kwamba Februari 6, 2023 kulikuwa na kuandika majina kwenye madawati ya wanafunzi hivyo walilazimika kukaa nje kusubiria na ndipo mwalimu huyo alitumia fursa ya kuwaingiza  darasani kuwakalisha chini kisha kuwapiga picha na  kurusha mitandaoni.

“Hali hiyo imezua taharuki kubwa kwetu viongozi wa mkoa na kulazimika kufanya ziara ya kushtukiza kuja kujionea hali halisi, ambapo tumekuta wanafunzi wakiendelea na masomo na kuwepo kwa idadi kubwa ya madawati katika shule hiyo,” amesema Malisa.

Afisa Elimu Mkoa wa Mbeya, Ernest Hinju amekemea kitendo hicho na kuweka bayana kuanza kwa utaratibu wa kuwachunguza walimu  wa muda wa kujitolea wanataka kufundisha kabla ya kupata nafasi Serikali huku akishindwa kuweka bayana kama mwalimu huyo ni mwajiriwa au la.

Naye, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya, Triphonia Kisiga amekemea tabia hiyo na kuonya walimu kuepuka tabia ya kuisemea vibaya Serikali kwa maslahi yao binafsi na kwamba kwa sasa licha ya kushikiliwa na Jeshi la Polisi pia amesimamishwa kazi.

Mume ahoji uhalali kesi ya kumuua mkewe
Juma Mgunda: Tumeisoma Horoya AC