Upande wa utetezi katika kesi ya mauaji, inayomkabili Khamis Luwongo maarufu Meshack anayetuhumiwa kumuua mkewe, umefungua shauri dogo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam wakihoji uhalali wa kesi hiyo.

Hayo yalibainishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na mawakili wa mshtakiwa Zidadi Mikidadi, Fatuma Abdalah na Mohamed Majaliwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Ramadhani Rugemalira.

Mawakili hao, kila mmoja kwa wakati wake mbali na mambo mengine, walidai uwepo wa kesi hiyo Namba 5 ya Mwaka 2022 unakwenda kinyume cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

Khamis Luwongo maarufu kama Meshack, akiwa chini ya ulinzi.

Mikidadi alidai mteja wao awali alikuwa akikabiliwa na kesi ya mauaji namba 72 ya mwaka 2020 ambayo upande wa mashitaka uliifuta na kufungua upya kesi hiyo yenye shitaka lilelile jambo ambalo sheria inataka likifanyika kesi ianze kusikilizwa mara moja.

“Kwa mujibu wa sheria hii, mshitakiwa akifutiwa kesi halafu akafunguliwa upya yenye mashitaka yaleyale inatakiwa isikilizwe haraka, lakini kesi hii mpya tangu ifunguliwe imeshaletwa mara tano na hakuna kinachoendelea wanasema upelelezi haujakamilika,” alidai.

Kutokana na hali hiyo, wamepeleka maombi Mahakama Kuu kupitia uhalali wa kesi hiyo kuendelea kuwepo mahakamani kwa sababu imekiuka sheria huku akidai shauri hilo dogo namba 186 ya mwaka 2022, litatajwa kwa mara ya kwanza Machi 20, mwaka huu mbele ya Jaji Obadia Bwegoge.

Naomi Marijani, katika picha mbili tofauti enzi za uhai wake na tangazo lililotolewa akitafutwa kulia.

Awali, Wakili wa Serikali, Mosie Kaima alidai kesi hiyo ilipelekwa mahakamani hapo kutajwa na kwamba bado wapo katika hatua ya kuwasilisha jalada Mahakama Kuu na ndipo hoja hiyo ya upande wa utetezi ilipoibuka na kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 28, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.

Luwongo ambaye ni mkazi wa Kigamboni, Dar es Salaam anadaiwa kumuua mkewe Naomi Marijani, Mei 15, 2019, katika eneo la Gezaulole wilayani Kigamboni kwa kumchoma moto kwa kutumia magunia mawili ya mkaa, kisha kufukia majivu shambani kwake na kupanda mgomba juu yake.

Serikali yabainisha mikakati kupambana na Fistula
Mbaroni kwa kuwakalisha chini Wanafunzi, kuwapiga picha