Mwenyekiti mwenza wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), James Mbatia ameomba kufanyika mdahalo kati ya vyama vinavyounda umoja huo na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Mbatia alitoa ombi hilo jana usiku katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam ambapo aliwasihi viongozi wa CCM kuwachagua wasemaji wao ili waweze kujumuika pamoja katika mdahalo kwa lengo la kunadi sera na ilani za vyama vyao.

“Tunawataka CCM wachague msemaji wao, na kwa kuwa Ukawa haitambuliki kama chama cha siasa, vyama vyote vya upinzani vitaweka wasemaje wao, ili tuache porojo na maneno maneno,” alisema Mbatia na kuongeza kuwa vyama ndivyo vinavyowakilisha mfumo wa serikali inayotarajiwa na sio mtu mmoja.

Kadhalika, Mbatia ambaye ni mwenyekiti wa NCCR – Mageuzi alizungumzia taarifa zilizoeleza kuwa mgombea wa Chadema aliomba kura kanisani. Alisema habari hizo ni za uongo kwa kuwa Lowassa aliwaomba waumini wa dini yake kumuombea na sio kumpigia kura. Alisema Lowassa sio mshirikina na ndio sababu amemtanguliza Mungu kwenye kampeni zake.

Aidha, alieleza kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) walipaswa kumkemea mgombea wa CCM, Dk John Magufuli kwa kauli yake kuwa mabadiliko yanaweza kuisababishia nchi matatizo kama ya Libya. Alisema badala ya kumkemea NEC iliwaeleza kuwa kauli hiyo ni ‘vionjo vya kisiasa’. Alisema kauli hiyo haikuwa kauli ya busara kwa kuwa ililenga katika kuwashawishi wananchi kwa kuwatishia hali ya usalama.

Katika hatua nyingine, Mbatia alimkosoa mgombea urais wa CCM kwa kile alichodai kuwa anataka kujitenganisha chama chake ili aonekane kuwa yeye sio chama katika kukwepa kubeba majukumu ya maswali ya watanzania kwa chama hicho.

“CCM ni Magufuli na Magufuli ni CCM, watanzania msirubunike,” alisema Mbatia akitoa mfano wa mabango ya mgombea huyo kuwa hivi sasa yameandikwa ‘Chagua Magufuli’ huku yakikitenga chama tofauti na miaka iliyopita ambapo wananchi walihimizwa kuchagua Chama sio mtu.

Ni Kusuka Ama Kunyoa Kwa TP Mazembe
Lowassa Kuwakabidhi Wananchi Kiwanda Cha Mtibwa