Mkaguzi Kata wa Kata ya Makuro Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Balumu S. Saguda ameweka bayana mbinu zinazotumiwa na wahalifu kufanya ukatili na unyanyasaji kwa watoto ikiwemo kuwapatia zawadi ndogondogo kama Pipi, Biskuti, Pesa na kufanikisha malengo yao ambayo ni maovu.
Saguda ameyabainisha hayo wakati alipokuwa anatoa elimu ya ushirikishwaji wa Jamii kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Mikuyu iliyopo Kijiji cha Mikuyu, Kata ya Makuro, Tarafa ya Mtinko, Manispaa ya Singida.
Pamoja na elimu hiyo, amewaelekeza watoto jinsi ya kutoa taarifa za ukatili kwa Jeshi la Polisi, kwa uongozi wa Serikali za Mitaa na kwa wadau wengine wa kupinga ukatili pindi wanapofanyiwa au kuona wengine wakifanyiwa vitendo hivyo ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma zao.
Katika hatua nyingine, Mtandao wa Polisi wanawake Wilaya ya Kigamboni wametoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Kisarawe II ikiwa ni katika kuelekea maadhimisho za siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika viwanja vya shule hiyo iliyopo Manispaa ya Kigamboni.