Mshambuliaji wa Simba SC, Meddie Kagere amesema anamuhofia mshambuliaji wa Azam FC, Prince Dube katika mbio za kuwania tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara (VPL) msimu huu 2020/21.
Kagere ametoa kauli hiyo, kufuatia ushindani uliopo kwenye orodha ya ufungaji bora kwa sasa, ambapo idadi ya mabao kati yake na mshambuliaji huyo kutoka nchini Zimbabwe inakaribiana sana.
Mshambuliaji huyo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Simba SC kwenye mchezo wa jana Jumapili dhidi ya Mwadui FC mjini Shinyanga, amesema Dube amekua akifanya vizuri kwa kutumia nafasi anazozipata akiwa uwanjani, hivyo hana budi kumuhofia.
Hata hivyo Mshambuliaji huyo kutoka nchini Rwanda, amesema pamoja na changamoto hizo amejipanga kukabiliana nazo na kuzishinda kwa kufunga mabao kila atakapopewa nafasi ya kucheza hata kama ni dakika 10.
“Dube ndiye ninayemhofia kwenye mbio za ufungaji bora msimu huu, sababu amekuwa akifanya vizuri kila anapopata nafasi ya kucheza kwenye timu yake na bahati mbaya kwangu msimu huu sipati muda mrefu wa kucheza,” amesema Kagere.
Kagere anaongoza katika orodha ya upachikaji mabao VPL kwa kufikisha mabao 11, akifuatiwa na Prince Dube mwenye mabao 10.