Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe amemuandikia barua Rais wa Tanzania, John Magufuli akimtaka kufuta uchaguzi wa Serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, 2019 kuanza mchakato wa maridhiano ya kitaifa.
Mbowe ameeleza hayo leo, Jumatatu Februari 3, 2020, wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam na kubainisha kuwa kufutwa kwa uchaguzi huo kutathibitisha kuwa uchaguzi mkuu ujao utakuwa wa huru na haki.
“Kufutwa kwa uchaguzi huu kutahalalisha kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa huru na haki, uchaguzi huu utafanyika sambamba na uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais” Amesema Mwenyekiti huyo.
Ametuma barua Ikulu kwa Rais Januari 29, 2020 na kuomba mambo matatu likiwemo la marekebisho ya katiba yatakayo zaa tume huru ya uchaguzi.
Amesema mambo hayo matatu yasipo shughulikiwa, Chadema isilaumiwe kwa yatakayo tokea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020.
” Huu ni mwaka wa uchaguzi, kwa hali ilivyo kuna kila aina ya kiashiria cha kutokea machafuko ya kisiasa kama hatutazika viburi vyetu vya kiitikadi na kusimama pamoja” Amesema Mbowe.
Hali kadhalika amekumbusha wito wake wa kutaka maridhiano alioutoa Desemba 9, 2019 Jijini Mwanza katika maadhimisho ya miaka 58 ya Uhuru wa Tanganyika katika uwanja wa CCM.
Pia amesema “Ukimya wetu sio woga, tuna wanachama wengi tunaofanya kazi ya ziada kuwatuliza, subira haina mwisho siku yakifika yakufika tusilaumiane”.