Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amethibitisha kuwa mwanaye wa kiume, Dudley ameathirika na virusi vipya vya corona (Covid-19).
Kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, Mbowe amesema kuwa mwanaye huyo hakuwahi kusafiri nje ya nchi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na amepata virusi vya corona akiwa ndani ya jiji la Dar es Salaam.
“Mama yake ambaye ni daktari alipobaini hali hiyo alizitaarifu Mamlaka za Serikali zinazoshughulikia janga hili, nazo zilimtaka kijana apelekwe Hospitali ya Mwananyamala, Dar es Salaam kwenye vipimo zaidi ambapo alithibitika rasmi kuwa ana virusi vya corona,” ameeleza Mbowe kwenye taarifa yake.
Ameeleza kuwa amepata ushirikiano kadiri iwezekanavyo kutoka kwa Serikali kupitia timu iliyoongozwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Katibu wa Wizara na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, familia yake na marafiki waliokuwa karibu na mwanaye kwa kipindi cha hivi karibuni wamepewa ushauri na kuchukuliwa vipimo.
Amesema Dudley amewekwa kwenye uangalizi maalum (karantini) akiendelea kupata matibabu na hali yake inaimarika.