Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe, amesema kuwa chama hicho wanahujumiwa huku akilaani Jeshi la Polisi Mkoani Geita kwa kumkamata Waziri Mkuu wa Zamani aliyejiuzuru, Edward Lowassa.
Ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Kamati Kuu ya Chama hicho kilichofanyika Jijini Mwanza ikiwa ni siku moja mara baada ya kukamatwa kwa Lowassa.
Lowassa alikamatwa na polisi mkoani humo baada ya kuwasili akitokea mkoani Kagera kwa shughuli za kisiasa akiwa na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu.
“Jeshi la Polisi linaingilia shughuli zetu halali za kisiasa, limekuwa likifanya hujuma kwa chama chetu hasa kwa viongozi jambo ambalo halikubariki,”amesema Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe amemtaja Profesa Mwesigwa Baregu kuwa alikuwa miongoni mwa waliokamatwa baada ya mwanasiasa huyo kusimama ili awasalimie wananchi waliosimama barabarani.