Wananchi wa Kata ya Malolo iliyopo Jimbo la Kibakwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa wamemuomba Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene kusaidia ubadilishaji wa mchakato wa kuwapata walengwa halisi wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii – TASAF.
Ombi hilo lilitolewa kwa nyakati tofauti wakati wa mikutano ya hadhara ya Waziri huyo inayoendelea katika Vijiji vya Jimbo la Kibakwe, wakisema utaratibu uliopo umegubikwa na ubabaishaji na hivyo kutaka uainishaji wa walengwa ufanyike kwa uwazi ikiwezekana kupitia mikutano ya hadhara, ili waweze kuwapata wahusika halisi.
Wamesema, licha ya TASAF kuwashirikisha viongozi wa vijiji husika katika kuwabaini Walenga halisi, bado hawaridhishwi na jinsi mchakato unavyoendeshwa kwani kuwekuwa na usiri wa hali ya juu na katika ngazi za vijiji haufanyiki vizuri, hivyo kupelekea wasio maskini kuwa wanufaika na wahusika kuendelea kutaabika.
Akijibu malalamiko hayo, Waziri Simbachawene amesema tayari ameshatoa maelekezo kwa Menejimenti ya TASAF Makao Makuu, kuangalia namna bora ya kuwapata walengwa halisi wa Mpango huo huku wanannchi hao wakitaka walengwa wa Mpango huo ambao tayari wameimarika kiuchumi kuwa na utu kwa kujiondoa na kuwapisha wengine wanaostahili kuingizwa kwenye Mpango.