Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani limetangaza kumsamehe Mchungaji wa Usharika wa Kijitonyama, Dkt. Eliona Kimaro.
Askofu Dkt. Alex Malasusa ameyasema hayo hii leo Februari 19, 2023 katika ibada iliyofanyika Tabata, Jijini Dar es Salaam.
“Mchungaji Kimaro endelea kutafakari, endelea kukaa karibu na Mungu wako,” amesema Askofu Malasusa huku akiwaomba waumini na washirika mbalimbali kuwatunza na kuwaombea wachungaji wao.
Naye, Mchungaji Kimaro ameomba radhi kwa Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), Dkt. Fredrick Shoo kwa usumbufu wowote uliojitokeza wakati huu ambao amekuwa likizo.
“Naomba radhi kwa mkuu wa kanisa Askofu, Dk Fredrick Shoo kwa usumbufu wowote ambao ulijitokeza katika mitandao na kwenye vyombo vya habari kwa wakati huu ambao nimekuwa likizo ya faragha,” amesema Dk Kimaro.
Itakumbukwa Januari 16, 2023 ilisambaa video ikimuonyesha mchungaji Kimaro akiwaeleza waumini wake kuwa amepewa likizo ya siku 60 baada ya kuitwa katika ofisi ya msaidizi wa askofu na kufanya kikao na mkuu wa jimbo.
Likizo hiyo ilikuwa inamalizika Machi 17, 2023 na Mchungaji Kimaro alipokuwa akiwaaga Washirika wa Kijitonyama alisema baada ya likizo hiyo hatarudi hapo, alielezwa akaripoti Makao Makuu ya Dayosisi.