Mbunge wa Kawe jijini Dar es salaam, Halima Mdee amemkaribisha na kumtahadharisha aliyekuwa Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro Nyalandu akimtaka ajiandae kisaikolojia kupambana na changamoto wanazokumbana nazo viongozi wa Chadema.
Ameyasema hayo kupitia mtandao wake wa kijamii wa Twitter kumkaribisha nadani ya chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) mara baada ya kutangaza kukihama Chama cha Mapinduzi (CCM) na kujiuzulu nafasi ya Ubunge.
“Mhe. Nyalandu karibu sana CHADEMA. Naamini utakuwa imara kukabiliana na siasa za chuki, ubaguzi na visasi zinazolikabili taifa letu, hivyo naimani umechukua maamuzi mazuri ila jiandae kukabiliana na changamoto,”amesema Mdee
Hata hivyo, mapema leo Nyalandu ambaye alikuwa Mbunge wa Singida Kaskazini na Mjumbe wa Halmashauri ya Kamati Kuu CCM alitangaza kujiuzulu nafasi zake hizo kwa kile alichodai kwamba hafurahishwi na mambo ya kisiasa yanayoendelea nchini na kuwaomba wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo kama wataridhia wampe nafasi ili kuweza kuleta mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi kupitia chama hicho.