Shirikisho la Soka nchini Tanzania TFF limemtangaza mshambuliaji wa klabu bingwa Tanzania bara Simba SC Meddie Kagere kuwa mchezaji bora wa mwezi Agosti katika Ligi Kuu msimu wa 2018/19.
Kagere amekuwa mchezaji wa kwanza katika msimu huu wa 2018/19 kushinda tuzo hiyo ambayo hutolewa kila baada ya mwezi mmoja.
Mshambuliaji huyo kutoka nchini Rwanda ameisaidia Simba kujikusanyia alama 6 za Ligi Kuu kupitia michezo dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City huku akifunga mabao matatu.
Kagere ametwaa tuzo hiyo kwa kuwashinda wapinzani wake wawili, Joseph Mahundi wa Azam na Ompar Mponda wa Kagera Sugar alioingia nao fainali ambao kila mmoja alifunga mabao mawili mwezi huo.
Kihistoria, Kagere aliibukia Mbale Heroes FC ya kwao, Uganda mwaka 2004 ambako alicheza hadi mwaka 2006 alipohamia Rwanda.
Klabu yake ya kwanza ilikuwa ni ATRACO FC alikocheza kwa msimu mmoja kabla ya mwaka 2007 kuhamia Kiyovu Sports alikodumu hadi 2008 akahamia Mukura Victory ambako alidumu hadi 2010 alipojiunga na Polisi.
Na akiwa Polisi ndipo akashawishiwa kuchukua uraia wa Rwanda ili achezee timu ya taifa ya nchi hyo jambo ambalo alilikubali na tangu mwaka 2011 amekuwa akiichezea Amavubi. Polisi alidumu kwa miaka miwili kabla ya mwaka 2012 kuchukuliwa Esperance Sportive de Zarzis ya Tunisia.
Alicheza Tunisia kwa mwaka mmoja kabla ya kurejea Rwanda kujiunga tena na Polisi mwaka 2013 ambako alicheza kwa mwaka mmoja na kuhamia Rayon mwaka 2014 ambayo mwaka 2015 ilimuuza KF Tirana ya Albania alikocheza hadi mwaka 2015 akajiunga na Gor Mahia ambako ameondoka Julai kuja Simba SC.