Mshambuliaji kutoka nchini Rwanda na Klabu ya Singida Big Stars Meddie Kagere amesema kwa sasa Young Africans ina Kikosi Bora kinachoundwa na wachezaji wenye umahiri mkubwa.
Kagere ametoa kauli hiyo baada ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa jana Alhamis (Novemba 17), Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Singida Big Stars ilikubali kupoteza kwa kufungwa 4-1.
Mshambuliaji huyo ambaye ameacha historia kubwa Simba SC kabla ya kuondoka mwanzoni mwa msimu huu 2022/23, amesema Young Africans imeendelea kuimarika tofauti na ilivyokua msimu uliopita ambayo alikutana nayo akiwa Msimbazi.
“Young Africans inaendelea kuwa tishio katika Ligi ya Tanzania Bara, wachezaji wake wanaimarika siku hadi siku, tumecheza nao leo (jana), imedhihiri wapo vizuri kwa sababu walituzidi kiuwezo.”
“Msimu uliopita walikua na timu nzuri, lakini hii ya msimu huu imeendelea kuwa Bora zaidi, wakiendelea hivi ninaamini wataweza kutetea Ubingwa wa Tanzania Bara kwa mara ya pili mfululizo.” amesema Mshambuliaji huyo
Mabao ya Young Africans katika mchezo dhidi ya Singida Big Starts yaliwekwa kambani na Mshambuliaji kutoka DR Congo Fiston Kalala Mayele aliyefunga matatu na Beki wa Kulia Shomari Kibwana, huku Meddie Kagere akifunga bao kufutia machozi.