Mabingwa wa Soka Tanzania Bara, Simba SC, wametoa sababu za kwenda mapema jijini Mwanza, kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Polisi Tanzania FC.
Kikosi cha Simba SC kiliwasili Mwanza jana Jumatano (Juni 17), kikitokea jijini Dar es salaam, na kinaendelea na maandalizi yake ya mwisho kuelekea mchezo huo utakaochezwa keshokutwa Jumamosi (Juni 19), Uwanja wa CCM Kirumba.
Meneja Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Patrick Rweyemamu amesema wameamua kwenda mapema jijini Mwanza kutokana na wachezaji wengi kuwa kwenye timu za Taifa, hivyo kwa muda watakaotumia jijini humo itarahisisha benchi la ufundi kupata muunganiko.
Amesema timu imeingia Mwanza na wachezaji 24, huku nyota watatu pekee, Ibrahim Ajibu, Jonas Mkude na Clatous Chama ndio wameachwa kutokana na matatizo binafsi.
“Ajibu ana mambo yake ya kifamilia, Mkude ishu zake zinajulikana lakini pia Chama alipatwa msiba, tumewahi Mwanza kuhakikisha tunashinda mechi hiyo japokuwa tunafahamu utakuwa mgumu” amesema Rweyemamu.
Simba SC inajiandaa kucheza dhidi ya Polisi Tanzania FC, huku ikiwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kumiliki alama 67, baada ya kucheza michezo 27.
Upande wa Polisi Tanzania FC wanakwenda kucheza dhidi ya mabingwa hao watetezi, wakiwa katika nafasi ya saba, kwa kumiliki 41 katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.