Hatimaye Serikali imefunguka kuhusu Uchaguzi Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini ‘TFF’ uliopangwa kufanyika Agosti 7, mkoani Tanga.

Wadau wa Soka walikua wakisubiri kauli ya Serikali, kufuatia baadhi yao kulalamikia kanuni za Uchaguzi huo, ikiwamo kipengele cha kupata wadhamini angalau kuanzia watano wakidai hakina usawa kwa wagombea.

Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Ally Possi amesema mchakato huo utaendelea kwa kanuni na taratibu za TFF.

“Kamati ya uchaguzi imefafanua kila kitu, hivyo uchaguzi wa TFF utafanyika kwa kanuni na taratibu za shirikisho hilo,” amesema.

Kwa upande wa Kaimu Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Taifa ‘BMT’, Neema Msita ameeleza kupokea baruapepe kutoka kwa mdau wa soka akilalamikia baadhi ya vipengele kwenye Katiba ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

“BMT ni chombo kilichoanzishwa kwa mujibu wa sheria na kipo kwa ajili ya kusimamia vyama, klabu pamoja na shirikisho zote za michezo nchini na tumekuwa tukihakikisha kwa kuona vyama na klabu zikijiendesha kwa kuzingatia katiba.

“Tunaelewa sasa hivi vyama vingi pamoja na klabu zinaendelea na uchaguzi ikiwemo TFF, hivyo wito wetu kwa shirikisho na wadau wote kuhakikisha wanafanya mambo yao kwa kufuata katiba,” alisema Neema.

Ameongeza kama kutatokea makosa yoyote vyombo vya serikali vipo macho na wasisite kutoa taarifa ili kuona haki inatendeka.

Amesema wao wanaisajili katiba baada ya kupata maoni ya wadau, hivyo yanapojitokeza maoni ya namna hii wana mamlaka ya kutengua baadhi ya vitu wakati wa usajili wa katiba.

Mgongolwa atoa afafanua uchaguzi TFF
Hati ya mashaka yawafukuzisha kazi watumishi 6 Kilimanjaro