Joseph Armand Bombardier ni mvumbuzi na mfanyabiashara mwenye asili ya Ufaransa na Canada ambaye ndiye mwanzilishi wa Kampuni ya Bombardier.
Moja ya vitu vilivyompa umaarufu Joseph Bombardier, ni kuunda gari zenye uwezo wa kutembea juu ya barafu zilizofahamika kama ‘Snowmobile’.
Amepata ujuzi wa mambo ya makanika tangu akiwa mdogo kwa kujifunza kutengeneza na kurekebisha magari na akiwa na umri wa miaka 19 alifanikiwa kufungua Gereji yake binafsi ambayo aliita Bombardier.
Kutokana na changamoto ya kujaa barafu katika barabara wakati wa baridi na hali hiyo kupelekea watu kutoendesha magari yao, Joseph Bombardier aliona fursa na kuanza kuunda magari yenye uwezo wa kutembea juu ya barafu.
Sambamba na hilo moja ya sababu zilizo msukuma katika wazo lake la kutengeneza magari hayo ni baada ya mtoto wake kufariki baada ya kuumwa ugonjwa wa ‘Peritonitis’ na kushindwa kumfikisha Hospitalini kutokana na barabara kujaa barafu.
Hata hivyo mahitaji ya magari yalipungua baada ya Canada kujiingiza katika vita ya pili ya Dunia. Mwaka 1948 Joseph Bombardier aliyumba zaidi kibiashara baada ya Serikali kuanza kuondoa barafu katika barabara kuu.
Mwaka 2000 Joseph Bombardier alipewa utambulisho wa heshima kama mmoja wa wanasayansi na waandisi maarufu nchini Canada.
Joseph Bombardier alizaliwa April 16 mwaka 1907 na kufariki Februari 18, 1964 kwa ugonjwa wa Kansa akiwa na umri wa miaka 56 biashara yake ikiwa imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kuuza magari zaidi ya 8200 kila mwaka.
Mpaka anafariki Kampuni yake ilikuwa tayari imeingiza kiasi cha pesa inayofikia Dola za Canada 20 Milioni ambayo ni sawa na Dola za Canada 160 Milioni kwa mwaka 2004.
Baada ya kufariki, Kampuni ya Bombardier iliongozwa na watoto wake ambao wameiboresha Kampuni ya Bombardier kwa kutumia vifaa vya kisasa.
Hadi sasa Kampuni hiyo ambayo inajihusisha zaidi na utengenezaji vyombo vya usafirishaji, kama ndege na meli imezidi kuteka soko la kimataifa na moja ya wateja wao, ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo tayari imenunua ndege kutoka Bombardier.