Wasifu wa Raila Amolo Odinga Mwenyekiti wa chama cha ODM, mwanasiasa mkongwe ambaye mwaka huu anawania nafasi ya urais kwa mara ya tano, baada ya kutofanikiwa katika azma yake ya kuliongoza taifa hilo kwa mara nne, katika chaguzi za awali ambazo baadhi ziligubikwa na utata.
Raila Amolo Odinga, amekuwa katika safu ya siasa za Kenya kwa zaidi ya miongo mitatu, na anakumbukwa zaidi kama kiongozi wa upinzani wa muda mrefu, na ambaye azma yake ya kuiongoza Kenya mara kwa mara imepelekea matukio ya kihistoria yaliyobadilisha taswira ya siasa za nchi hiyo.
Kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022, itakuwa ni mara ya tano kwa Raila Odinga kuwania urais, na baadhi ya wachambuzi wanasema huenda hii ndiyo nafasi yake bora zaidi ya kupata ushindi, hususan baada ya rais anayeondoka Uhuru Kenyatta na ambaye kwa kipindi kirefu alikuwa hasimu wake wa kisiasa, kutangaza hadharani kwamba anaunga mgono azma ya Odinga kuwa rais wa tano wa Kenya.
Raila Odinga alizaliwa tarehe 7 Januari 1945, katika mji wa Maseno, wilaya ya Kisumu, nchini Kenya.
Baada ya masomo yake aliingia katika utumishi wa umma kwa mara ya kwanza mwaka 1974, na kushikilia nyadhifa mbalimbali katika shirika la ubora wa Viwango vya bidhaa la Kenya (KEBS), hadi mwaka 1982 alipoanza harakati zake za kisiasa akipinga utawala wa chama cha KANU, ambao ulionekana na wakosoaji kuwa wa kidikteta.
Kufuatia jaribio la kuipindua serikali ya Rais Daniel Toroitich Arap Moi, utawala wa Moi ulianza msako kwa lengo la kuwawajibisha waliohusika.
Odinga ni mmoja kati ya watu waliokamatwa, na baadaye akashtakiwa kwa uhaini na kutumikia vifungo viwili kwa karibu muongo mmoja.
Baada ya kuachiliwa Odinga alikimbia nchi na kutafuta hifadhi nchini Norway kwa hofu ya kukamatwa tena.
Alirejea Kenya na kujikita katika harakati za ukombozi kupitia Forum for the Restoration of Democracy (FORD).
Aliporudi kutoka uhamishoni, alijiingiza kikamilifu katika siasa, akiungana na babake Jaramogi Oginga Odinga, Makamu wa Rais wa zamani, na watetezi wengine kushinikiza Serikali ya Moi kufungua nafasi ya kidemokrasia nchini Kenya.
Wanaharaati hao, waliendelea kumtaka Rais Daniel Arap Moi, kuridhia msukumo wa kubadilisha kipengele cha katiba, kilichoifanya Kenya kuwa nchi ya mfumo wa chama kimoja cha kisiasa na hilo lilifanyika mwaka wa 1991.
Kupitia Forum for Restoration of Democracy (FORD), Raila alijitosa kwenye Siasa za kuchaguliwa mwaka 1992, alipogombea kiti cha ubunge katika eneo la Lang’ata, nje kidogo ya jiji kuu la Kenya, Nairobi.
Baadaye, mwaka 1997 alijitosa kwenye kinyang’anyiro cha urais bila mafanikio na aligombea tena mwaka 2007, 2013 na 2017, Odinga amekuwa mwanachama wa vyama vingi vya kisiasa tangu wakati huo.
Mnamo 2002, alijiunga na vyama vingine vyenye mawazo kama hayo kumfanyia kampeni Mwai Kibaki chini ya Muungano wa National Rainbow Alliance (NARC), muungano ambao hatimaye uliiondoa KANU serikalini na kuleta mapambazuko mapya katika nyanja ya kisiasa ya Kenya.
Akiwa mkosoaji mkubwa wa serikali katika enzi ya Moi, na baadaye marais Mwai Kibaki na Uhuru Kenyatta, Odinga amekuwa taswira ya siasa za upinzani nchini Kenya kwa kipindi kirefu na aliandika historia kama mwanasiasa wa kwanza aliyefaulu kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais, na kusababisha kufutwa kwa uchaguzi wa kwanza wa urais barani Afrika, hapo mwaka 2017.
Baada ya uchaguzi wa marudio wa mwaka 2017, ambao Odinga na wenzake katika muungano wa kisiasa uliopewa jina la NASA walikuwa wameususia, mwanasiasa huyo alipanga hafla ya kujiapisha kama kile alichokiita raisa wa wananchi, na hapo tarehe 30 mwezi Januari mwaka 2018, uapisha huo ukafanyika kwenye bustani za Uhuru Park mjini Nairobi.
Hata hivyo, jambo hili halikupokelewa vyema na serikali na kusababisha hali ya taharuki, maandamano, uporaji na mauaji, huku upinzani na Serikali zikiendelea kuchukua misimamo iliyohitilafiana.
Odinga, pia ameandika historia kwa kuwa sehemu ya mpango uliofeli wa kutafuta maridhiano ya kitaifa maarufu BBI, huku akipeana mikono na mpinzani wake wa miaka mingi Uhuru Kenyatta Machi 9, 2018, tukio ambalo halikutarajiwa na wengi na ambalo limeendelea kujadiliwa kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.
Odinga amesema mara kwa mara kwamba, iwapo atachaguliwa kama Rais mchakato huo wenye utata, ambao ulisitishwa na Mahakama ya juu, kwa kuwa haukufuata mkondo ufaao kwa mujibu wa katiba ya Kenya, utafufuliwa upya.
Disema 10, mwaka 2021 Odinga alitangaza kwamba atagombea urais wa Kenya, kauli mbiyu yake ikiwa ni kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini humo.
Chama chake cha ODM, kimeshirikiana na vyama vingine ikiwa ni pamoja na kile kinachotawala hivi sasa cha Jubilee, na kuunda muungano wa upinzani uitwao Azimio la Umoja One Kenya, ambao umeridhia apeperushe bendera yake kama mgombea urais.
Pamoja na kuwa mwanasiasa aliyebobea, Odinga pia ni Mwakilishi Mkuu wa Maendeleo ya Miundombinu katika Tume ya Muungano wa Afrika, nafasi anayoishikilia tangu mwaka 2018.
Iwapo atachaguliwa, Odinga atakuwa Rais aliyeingia madarakani akiwa na umri mkubwa zaidi, katika historia ya nchi hiyo.