George Wajackoyah, aliye katika mbio za kuwania Urais nchini Kenya, nyuma ya wapinzania wawili wenye nguvu Raila Odinga na William Ruto, chini ya kauli mbiu yake ya “ganja” amefanikiwa kupata umaarufu katika vyombo vya Habari ndani na nje ya nchi hiyo hasa wapiga kura vijana.

Moja ya vivutio katika kampeni zake, ni juu ya suala la matumizi ya bangi katika kuinua uchumi wa Taifa hilo akijinasibu kuwa Kenya itapiga hatua zaidi katika mapambano ya umasikini uliokithiri hasa baada ya vita ya Ukraine na uwepo wa maradhi ya Uviko-19.

Gwiji huyo wa muziki wa reggae, George Wajackoyah ameibuka kuwa mgombeaji ambaye ameahidi kufuta deni la nchi kwa suluhisho la bangi ambayo maeneo mengine imekuwa ikipigwa marufuku kutokana na kujumlishwa katika sehemu ya dawa za kulevya.

Prof. George Wajackoyah, Mgombea wa kiti cha Urais Nchini Kenya. (Picha na Zadock Thomas/eafeed).

Hata hivyo, Wajackoyah amewavutia wanachama wapya na wapiga kura wengi ambao wamekuwa na maoni tofauti juu ya kinachoendelea nchini Kenya wakisema wanasiasa wameshindwa kukabiliana na ufisadi, mfumuko wa bei na ukosefu wa ajira.

Wakati wa kampeni zake, Ganja man Wajackoyah ameahidi kufuta deni la karibu $70 bilioni za Kenya (sawa na pauni 57.9 bilioni), kwa kuanzisha sekta ya matibabu ya bangi na kusafirisha sehemu za wanyama hadi Uchina, ambapo anasema korodani za fisi pia zitauzwa kwa wingi na kuliingizia pato Taifa.

“Nimeunda kabila jipya, linalojulikana kama kabila la ganja,” aliwaambia wafuasi wake akielezea umaarufu wake wakati wa Kampeni zake maeneo kadhaa nchini Kenya.

Mgombea huyo, anagombea huku akiwa na bajeti ndogo huku wafuasi wake wakitengeneza mabango ya kawaida yaliyo na kauli mbiu “Wajackoya wa 5”, inayorejelea azma yake ya kuwa rais wa tano wa Kenya.

Wackojah anasema katika kampeni zake kuwa, “Nikikuonyesha kiasi cha pesa nilichonacho, ungecheka.” na kufanya shangwe kuibuka miongoni mwa wafuasi wake lakini akiwa na imani kwamba anaweza kuliongoza Taifa hilo na kulifikisha sehemu salama.

Katika mikutano yake, amekuwa akipiga muziki wa reggae kutoka kwenye gari lake na kuelekeza ugombea wake kwa watazamaji ambapo Agosti 3, 2022 msafara wa Wajakoyah ulienda Gatundu, karibu kilomita 30 kaskazini mwa mji mkuu na umati wa watu wapatao 400 walikusanyika.

“Kila mzunguko wa uchaguzi kila mtu huja hapa na propaganda zao, lakini ikiwa mtu huyu anaweza kufanya kile anachosema kweli basi tutafika mbali sana kama nchi,” ” alisema mmoja wa wafuasi wake Jeff Mwangi.

Taifa hilo tajiri katika eneo la ukanda wa Afrika Mashariki, litafanya uchaguzi wake Agosti 9, 2022 huku kiongozi mkongwe wa upinzani Raila Odinga na naibu rais William Ruto wakichuana vikali katika kinyang’anyiro hicho.

Prof. George Luchiri Wajackoyah almaarufu Wajackoyah wa Tano, ni miongoni mwa wagombeaji wanne wa urais katika uchaguzi mkuu wa Agosti 2022 na ni miongoni mwa Wakenya waliosoma zaidi akiwa na jumla ya digrii 17, ambapo anasema lengo lake ni kuhalalisha bangi nchini Kenya ili kulipa madeni ya nchi, iwapo atachaguliwa.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo August 7, 2022     
Amuuwa baba yake kwa kuoa mke wa pili