Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans upo kwenye harakati za kunasa saini ya mfumania nyavu mahiri wa klabu ya Cape Town inayoshiriki Ligi Kuu ya Soka ya Afrika Kusini, Khanyisa Mayo.

Mayo mwenye umri wa miaka 24 pia anawindwa na klabu za Kaizer Chiefs na Mamelodi Sundowns zote za Afrika Kusini ameingia katika kinyang’anyiro hicho baada ya kuifungia timu yake ya Cape Town mabao 12 kwenye ligi mpaka sasa akifungana na mshambuliaji nyota wa Sundowns, Mnamibia Peter Shalulile.

Mitandao mbalimbali ya kijamii ya Afrika Kusini jana Jumanne (Mei 16) vilifichua kuwa mabingwa wa Tanzania Bara, Young Africans na ambao wako nchini humo kucheza mchezo wa Mkondo wa Pili wa Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Marumo Gallants wameanza mazungumzo na nyota huyo mwenye umri wa miaka 24.

Mayo aliyeitwa kwa mara ya kwanza kuitumikia timu ya taifa Afrika Kusini, Septemba mwaka jana ambae hivi karibuni alipewa tuzo ya mchezaji bora wa timu yake anatazamwa na Young Africans kama mrithi sahihi wa Fiston Mayele ambaye anatajwa kuwa kwenye nafasi kubwa ya kuondoka kwa Wanajangwani hao mwishoni mwa msimu huu.

Taarifa za Mayo kutakiwa na Young Africans zilichagizwa zaidi na mahojiano ya rais wa klabu hiyo Hersi Said aliyofanya na moja ya Luninga za nchini humo.

“Nahitaji kusajili mchezaji mmoja kutoka Afrika Kusini kwa sababu za kiufundi sio za mashabiki. Tuna sababu nyingine wakati tunaposajili mchezaji, Young Africans ni maarufu sana Afrika nzima kutokana na wachezaji inaowasajili.

“Mfano tukicheza Congo kila mmoja anaishangilia Young Africans kwa sababu ya Fiston Mayele,” amesema Hersi akithibitisha kuwa wako mbioni kusajili mshambuliaji kutoka Afrika Kusini.

Simba SC yaanza na Edmund John, Mwanuke
Mahakama yataja sababu kumuachia huru Yesu