Katibu mkuu wizara ya habari, utamaduni, sanaa na michezo, Dkt. Hassan Abbasi, amesema kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuboresha mifumo ya hakimiliki ili kuhakikisha wasanii wa tasnia mbalimbali wananufaika katika kazi zao za ubunifu zinapotumika iwe kwenye redio, TV, mitandaoni na kila sehemu ya biashara.
Ameyasema hayo alipokutana na waandaaji wa muziki na filamu, DJ na wasambazaji wa kazi za sanaa ikiwa ni mikakati ya pamoja ya kutatua kero za sekta hiyo.
“Tangu Cosota ihamie Wizara ya Habari tumeendelea kuboresha mifumo ya ndani ya kiutendaji ikiwemo kuandaa mifumo mipya ya kimtandao kusajili kazi kiurahisi, kuboresha kanuni ili wanaokamatwa na kazi za wasanii watozwe faini papohapo” amesema Dkt Abassi
Hata hivyo wadau wa sekta ya sanaa pia wameomba kujengewa kumbi za maonesho na burudani na kupunguziwa utitiri wa kodi ambazo Abbasi amewataka waainishe kodi zenye kero ili zijengewe hoja na serikali.