Jeshi la polisi Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini (STPU) limekamata mifugo 314 katika maeneo ya kijiji cha Ngoyoni tarafa ya Mengwe wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro, ikiwa imeingizwa nchini kinyume cha taratibu.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia Wizi wa Mifugo nchini Simon Pasua amethibitisha kukamatwa kwa mifugo hiyo ambapo amesema, uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini mifugo hiyo imeingizwa nchini ikitokea nchi jirani kwa ajili ya kutafuta malisho.
Kamanda Pasua amesema katika siku za hivi karibuni kumejitokeza tabia ya baadhi ya wafugaji kutoka nje kuingiza mifugo na kulisha katika mashamba ya wakulima bila kujali kuwa mashamba hayo yana mazao na kufanya uharibifu mkubwa, hali inayosqbabisha migogoro baina ya wafugaji na wakulima.
Aidha ametoa onyo kwa wafugaji wote nchini wenye tabia ya kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima kuacha mara moja tabia hiyo, kwani hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Amesema, iko haja kwa wakulima na wafugaji kufuata taratibu za matumizi sahihi ya ardhi ili kuepusha migogoro kati ya wafugaji na wakulima isiyo ya lazima.