Ripoti mpya iliyotolewa hii leo Septemba 8, 2022 na Umoja wa Mataifa, kuhusu maendeleo ya binadamu inaonya kuwa migogoro mingi inazuia hatua za maendeleo ya binadamu, ambayo sasa inarudi nyuma katika nchi nyingi.
Ripoti hiyo ya maendeleo ya binadamu ya 2021/22 (HDR), ambayo imepewa jina la “Nyakati zisizo na uhakika, maisha ya misukosuko: Kuunda mustakabali wetu Katika ulimwengu unaobadilika” inatoa taswira ya jamii ya kimataifa inayohaha kutoka kwa mogogoro ambayo inahatarisha ongezeka la changamoto na ukosefu wa haki.
Kinachoongoza orodha ya matukio yanayosababisha usumbufu mkubwa duniani ni janga la Uviko-19 na uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, ambao umekuja huku kukiwa tayari na mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi, hatari ya sayari, na ongezeko kubwa la ubaguzi.
Kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 32, ambayo shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP), limekuwa likitoa tathimini ya maendeleo ya binadamu, inayopima afya ya taifa, elimu, kiwango cha maisha, maendeleo yameshuka duniani kwa miaka miwili mfululizo.