Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Innocent Bashungwa amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wilaya zote nchini kuwasimamia Wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Maafisa elimu, Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu, Wathibiti Ubora wa Shule kuhakikisha wanawafuata walimu mashuleni na kutatua kero zao kwa wakati.

Aidha, Bashungwa pia amepiga marufuku walimu kupita kila ofisi ya Halmashauri kutatua shida zao na kuagiza wapelekewe huduma hizo shuleni badala ya wahusika kufuatwa ofisini.

Akitoa agizo hilo hii leo Septemba 8, 2022 Jijini Dodoma wakati akiongea na waandishi wa habari, Bashungwa ametoa taarifa kwa umma juu ya uboreshaji wa huduma kwa walimu nchini.

Amesema, “Ni marufuku kuwaacha walimu kupita kila ofisi ya Halmashauri kutafuta huduma, narudia tena mwalimu apelekewe huduma shuleni badala ya watoa huduma kukaa ofisini.”

Hata hivyo, amewataka viongozi hao kufuatilia na kuwasimamia viongozi wa elimu katika ngazi ya Mikoa, Halmashauri, Kata na shule kutekeleza mikakati ya uboreshaji na usimamizi wa elimu na kuhakikisha wanawasilisha taarifa ya utekelezaji Ofisi ya Rais – TAMISEMI kila robo ya mwaka.

Ameongeza kuwa, viongozi hao wanatakiwa kusimamia utekelezaji wa Mipango ya Mafunzo kazini kwa walimu, kwa mujibu wa Mwongozo uliotolewa na Katibu Mkuu Utumishi na ufanyike kwa uwazi na ushirishwaji wa kutosha, ili kuondoa dhana ya kuwa waajiri wanatoa nafasi za mafunzo kwa upendeleo.

Katika hatua nyingine, Bashungwa pia amewaelekeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya, kuwasimamia Maafisa wa Tume ya Utumishi wa Walimu kuzingatia miongozo ya upandishwaji vyeo walimu, ili kila anayestahili kupandishwa cheo, anapandishwa kwa mujibu Sheria, Kanuni na Miongozo.

Hata hivyo, Bashungwa amesisitiza kuwa Mwalimu anapoandika barua kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhitaji huduma, anapaswa kujibiwa kwa maandishi ndani ya siku 7 baada ya kupokelewa na vinginevyo.

Putin aonesha dharau akitangaza kukutana na Xi
Wakili amtaka Waziri kutimiza ahadi mapendekezo ya wadau wa Habari