Wakili wa Kujitegemea James Marenga, amesema ahadi ya Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ya kupeleka mapendekezo ya wadau wa habari katika Bunge la mwezi Septemba inapaswa kutimizwa.

Kauli ya Wakili Marenga, ameitoa hii leo Septemba 8, 2022 ikiwa ni siku moja baada ya Waziri Nape kusema tayari sheria hiyo imepata kibali na hivyo Baraza la Mawaziri linajiandaa kuiwasilishwa bungeni.

Amesema, muswada huo wa sheria ambao unatarajiwa kuwasilishwa bungeni Septemba 13, 2022 unawafanya wadau wa Habari kuwa na kiu ya kona pia Waziri Nape anatimiza ahadi yake ya kuwasilisha mapendekezo kuhusu mabadiliko ya sheria za habari Bungeni.

Amesema, “Wadau wangependa kuoana ahadi ya Waziri Nape ya kupeleka Mabadiliko ya Sheria ya Huduma za Habari yanafanikiwa kwenye Bunge hili la mwezi Septemba mwaka huu ili mchakato wa mabadiliko hayo ukamilike.”

Wakili Marenga ameongeza kuwa, mjadala wa serikali na wadau wa Habari ulihusu Sheria ya Huduma za Habari 2016 na kwamba vipo baadhi ya vipengele ambavyo tayari wamekubaliana.

“Mjadala wa serikali na wadau ulihusu Sheria ya Huduma za Habari 2016, na yaliyojadiliwa ni mapendekezo ya wadau na yale ya serikali, kuna vipengele tulikubalia na vingine bado vipo kwenye mjadala,” ameongeza Marenga.

Novemba 16, 2016 ilisainiwa Sheria ya Huduma ya Habari iliyopitishwa na Bunge la 11 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la mkutano wa 5 jijini Dodoma Tanzania

Akizungumzia sheria ya kulinda taarifa binafsi za kimtandao, Wakili Marenga amesema, sheria hiyo si ya wadau wa habari pekee bali inawahusu watu wote hivyo ni vyema kuifuatilia na kujua muafaka wake.

TAMISEMI kutatua kero za Walimu kwa wakati
Waziri Mkuu awatembelea majeruhi shambulio la bomu