Kocha Mkuu wa Young Young Africans Miguel Angel Gamondi amesema kuwa hana hofu ya mchezo wao dhidi ya Azam FC huku akiwatahadharisha kuwa wasitegemee kuona akitumia mbinu alizozitumia walipokutana katika Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii.
Miamba hiyo ya soka jijini Dar es salaam itakutana Jumapili (Oktoba 22), Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya Jiji hilo.
Young Africans itaingia katika mchezo huo, ikiwa imetoka kuifunga Azam FC mabao 2-0 yaliyofungwa na Clement Mzize na Kennedy Musonda kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Gamondi amesema kuwa, kila mchezo kwake anakuja na mbinu na mfumo tofauti, ambao anaamini utampa ushindi, hivyo wapinzani wake wasitegemee kuingia na staili hiyo ya uchezaji iliyompa ushindi katika Ngao ya Jamii.
Gamondi amesema kuwa jeuri hiyo anaipata kutokana na ubora wa wachezaji wake wote, ambapo hamtegemei mchezaji mmoja pekee huku akiahidi kupata ushindi katika mchezo huo ili wakae kileleni mwa ligi.
Ameongeza kuwa wachezaji wake wote wapo fiti na tayari kwa ajili ya mchezo huo, na morali kubwa ya kupata matokeo mazuri ili wafanikishe malengo yao ya kutetea ubingwa huo wa ligi.
“Nikiri mchezo wetu wa ligi unaofuatia dhidi ya Azam FC ni mgumu, kutokana na wao kuhitaji kulipa kisasi cha mabao 2-0 tulipokutana katika Nusu Fainali ya Ngao ya Jamii.
“Wao wakijipanga kulipa kisasi, lakini sisi pia tumepanga kupata ushindi katika mchezo huo, nimefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mchezo huo ambao muhimu kwetu kupata ushindi.
Tayari nimewaambia wachezaji wangu umuhimu wa mchezo huu, ambao tunatakiwa kushinda na sio sare, sina hofu ya hilo” amesena Gamondi