Katika kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kukabiliana na maambukizi ya Virus Vya Ukimwi – VVU, Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) imetoa mchango wa Sh milioni 17 kufanikisha mbio za nyika (ATF Marathon) zilizofanyika mkoani Morogoro ikiwa ni muendelezo wa maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yanayofanyika mkoani humo kitaifa Disemba Mosi mwaka huu.
Akizungumzia ushiriki wa GGML katika mbio hizo za ATF Marathon zilizofanyika Morogoro Jumapili tarehe 26 Novemba 2023, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa GGML, Stephen Mhando alisema mchango huo ni moja ya jitihada za kampuni hiyo katika kuwahamasisha na kuwaelimisha wananchi juu ya ugonjwa huo na kuutokomeza ifikapo 2030.
“Ufadhili huu wa GGML unadhibitisha dhamira ya dhati ya kampuni yetu kudumisha uendelevu kwa watu wote. Kwamba tunalenga kuhakikisha kuwa jamii inayozunguka shughuli za mgodi wetu na hata walio nje ya Geita wanafaidika na uwepo wa kampuni hii.
“Fedha hizi tunaamini zitagusa moja kwa moja maisha ya watu wanaoishi na VVU… Geita ikiwa moja ya mikoa yenye idadi kubwa ya wachimbaji madini ikiwamo wasio na VVU pamoja na wenye VVU, kwetu sisi GGML ni vigumu kukwepa jukumu kama hilo la kuwajali watu wa aina hii na kuwawezesha kwa namna mbalimbali.”
Awali akizungumza katika hafla ya kuwapokea washiriki wa mbio hizo zilizofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari ya Morogoro iliyopo Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Wilson Charles aliipongeza GGML na wadau wengine kwa kuunga mkono mbio hizo.
“Napongeza juhudi zinazochukuliwa na wadau wetu ikiwamo GGML pamoja wananchi katika ushiriki wao kwenye Mbio za hizi za Nyika zinazolenga kutunisha Mfuko wa Udhibiti wa UKIMWI (ATF) na kuunga mkono sera ya ‘Tokomeza Ukimwi, Tanzania bila Ukimwi inawezekana,” alisema kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI, Mohamed Mchengerwa.
Alisema wananchi wanapaswa kushirikiana na Serikali katika kupambana na maambukizi mapya ya UKIMWI ambayo hupunguza kasi ya maendeleo ya Taifa na kuongeza kuwa, “nipende kuwapongeza kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizi kwani mmeonekana mmeguswa na mna nia ya kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha malengo ya kutokomeza maambukizi ya virusi vya UKIMWI ifikapo mwaka 2030 yanafanikiwa.”
Kwa upande wake, Mshiriki wa ATF Marathon, Neema Matheo alisema kuwa mazoezi ni muhimu kwa mwili wa mwanadamu kwani bila mazoezi mwili huweza kupata magonjwa yasiyoambukiza kwa haraka na urahisi zaidi yakiwemo ugonjwa wa Moyo na Kisukari.
Katika mbio hizo mshindi wa kwanza wa kilomita 21 alipata zawadi ya Sh 300,000, mshindi wa pili Sh 250,000 na wa tatu Sh 200,000 vivyo hivyo kwa upande wa washindi wa mbio za baiskeli km 66.
Maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani, mwaka huu kitaifa yanafanyika mkoani Morogoro, yakiongozwa na kauli mbiu isemayo “Jamii iongoze kutokomeza Ukimwi”. Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo anatarajiwa kuwa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.