Ukuta unaozunguka Migodi ya Tanzanite Mirerani wenye urefu wa kilomita 24.5 umefungiwa jumla ya kamera 306 za usalama zenye uwezo wa kufanya kazi katika mazingira yoyote ikiwemo kumbaini mhalifu.
Kamera hizo zimewekwa kufuatia kuwepo umuhimu wa eneo husika kufungwa mfumo wa CCTV kwa lengo la kugundua vitu na watu wanaoingia eneo la ukuta, kuhifadhi taarifa za kudumu, kuzuia wanaokusudia kufanya uhalifu na kufuatilia matukio yanayofanyika eneo la ukuta huo.
Akikabidhi mfumo huo kwa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amesema kamera hizo zina uwezo wa kurekodi matukio wakati wa usiku, mchana, wakati wa jua, kwenye vumbi, wakati wa mvua na zina uwezo wa kumtambua mhalifu aliyekwishafanya uhalifu kwenye Ukuta.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Faraji Mnyepe akipokea Mfumo huo, amesema yapo manufaa yanayotokana na kufungwa kwa kamera hizo ikiwemo kukuza Pato la Taifa kutokana na udhibiti uliokuwa unafanywa wasio waaminifu.
“Shahidi wa hili ni bilionea Saniniu Lazier, tulimlinda tangu kuzalisha hadi anauza madini yake. Tunawaomba Wananchi na watanzania wote kulinda Madini Yetu, rasilimali ni jukumu letu wote. Ni malengo yangu wananchi wa Mirerani mtatusaidia kulinda Rasilimali hii,” amesema Dkt. Mnyepe.
Mbali na kukabidhi mfumo huo, Afisa Mahusiano na Mawasiliano wa Kampuni ya StarFix iliyofunga kamera hizo Jason Kyando, amesema kuwa baada ya zoezi la kufunga mfumo kukamilika walitoa mafunzo kwa wasimamizi wa mfumo huo ambao wote ni vijana wa Kitanzania kuhusu namna ya kusimamia mfumo huo.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila mradi huo uliosimamiwa na Kampuni ya Starfix Enterprise, umegharimu Shilingi Bilioni 1.2 na mpaka kukamilika uwekaji wa miundombinu yote iliyopangwakuwekwa ikiwa ni pamoja na ujenzi wa Scanner katika geti kuu la kuingia, uwekezaji huo kwa pamoja utakuwa umegharimu takriban shilingi bilioni 4.2.