Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya dharura, OCHA, Martin Griffiths ameeleza kusikitishwa kwake na kuondolewa kwa nguvu kwa meli za mafuta kutoka katika maghala ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa chakula duniani WFP huko Mekelle, Tigray nchini Ethiopia.
Kupitia taarifa yake iliyotolewa jijini New York Marekani, Griffiths amesema Meli 12 zilizokuwa zimebeba zaidi ya lita 570,000 za mafuta zilikusudiwa kusaidia Umoja wa Mataifa na washirika wake kusambaza vifaa vya misaada ya kibinadamu kwa watu ambao wanahitaji msaada.
Amesema, “Bila misaada hiyo watu wataachwa bila chakula, virutubisho vya lishe, madawa na vitu vingine muhimu. Wakati ambapo utapiamlo na uhaba wa chakula unaongezeka, matokeo yanaweza kuwa mabaya.”
Hata hivyo, amelaani utoroshwaji wowote wa mali za misaada na kusema, “ Usambazaji wa misaada ya kibinadamu lazima ulindwe kote Ethiopia na uzuiaji wa misaada ya kibinadamu lazima ukomeshwe.”
Kupitia taarifa hiyo, pia amerejea kutoa wito wa kurejesha huduma za kimsingi huko Tigray, ikiwa ni pamoja na huduma za benki na mifumo ya umeme, ambayo inaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha hali ya usaidizi wa kibinadamu katika eneo hilo.
Agosti 25, 2022, Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani (WFP), David Beasley alitoa taarifa ya kuitaka mamlaka ya Tigrayan kurejesha mara moja akiba ya mafuta iliyoibiwa kwa jumuiya ya kibinadamu.
Beasley alisema, kundi la watu wenye silaha waliingia katika ghala la WFP huko eneo la Mekelle na kukamata kwa nguvu meli 12 zilizojaa zaidi ya lita nusu milioni za mafuta.