Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewahakikishia Watanzania kuwa, Mamlaka ya Mapato Tanzania – TRA, itaendelea kusimamia masuala ya mapato Serikalini, kutoka kwa mwekezaji kwa mujibu wa sheria na taratibu za mikataba na kwamba itasimamia maoni yote yaliyotolewa.
Majaliwa ameyasema hayo hii leo Juni 28, 2023 Bungeni jijini Dodoma na kuongeza kuwa makubaliano ya uendeshaji wa Bandari kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai yanalenga kuweka msingi wa ushirikiano baina ya nchio hizo.
Amesema, maeneo ya uwekezaji yatakayopendekezwa ndiyo yatakayoingia mikataba kwa kila eneo na hivyo masuala ya mfumo wa uwekezaji kwa kutumika sheria za nchi na mgawanyo wa mapato utazingatiwa, huku muda wa uwekezaji na ukomo wa uwekezaji pia utajadiliwa.
“Bandari ya Dar es Salaam ndio kitovu cha huduma za bandari hapa nchini Ili kuiwezesha bandari hii kufanya kazi kwa ufanisi, kuongeza mapato ya nchi, ajira na kuchagiza sekta nyingine kiuchumi, serikali iliamua kutafuta kampuni yenye uwezo na uzoefu mkubwa katika uendeshaji wa bandari duniani kote teknolojia za kisasa,” amesema Waziri Mkuu.
Hata hivyo amesema, “kupitia sheria ya bandari ya mwaka 2004, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ndio iliyopewa mamlaka na haki ya kumiliki wa maeneo yote ya bandari nchini. Hakuna chombo chochote wala mamlaka ya bandari ambayo ina uwezo wa kutoa umiliki huo kwa kampuni yoyote ile.”