Mvutano mkubwa unaoendelea nchini Zimbabwe hususan katika chama tawala cha Zanu- PF kuhusu mrithi wa Rais Robert Mugabe umeibua mazito baada ya mkewe, Mama Grace kudai ameshtukia mpango wa mapinduzi na mauaji.
Mama Grace ameeleza kuwa timu ya Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Emmerson Mnangagwa ambayo inataka amrithi Mugabe imepanga kufanya mapinduzi na kuwaua wote watakaopinga utawala wake.
Akizungumza katika tukio lililofanyika jijini Harare, Mama Grace ambaye pia anataka kumrithi Mugabe alitahadharisha kuwa mpango huo hautafanikiwa kwani Jumuiya za Kimataifa hazitautambua utawala utakaoingia kwa njia hiyo.
“Tunatishiwa usiku na mchana kuwa kama mtu fulani hatakuwa Rais tutauawa. Hatutasujudia vitisho hivyo. Wanasema watafanya mapinduzi, lakini hakuna atakayewatambua. Umoja wa Afrika hautawatambua, SADC pia hawatawatambua,” BBC inamkariri Mama Grace.
Akizungumzia tuhuma dhidi yake kuwa alihusika katika mpango wa jaribio la kumuua Mnangagwa kwa kumlisha sumu kupitia ‘ice cream’ iliyotengenezwa na kampuni yake, Mama Grace alikanusha vikali madai hayo.
“Kwanini kampuni yangu itengeneze kikombe kimoja tu cha ice cream chenye sumu kwa ajili ya mtu mmoja? Kwanini nitake kumuua? Mimi ni mke wa Rais. Sasa huyo Mnangagwa ni nani? Nataka nini kwake?,” Alihoji.
Mnangagwa alikimbizwa hospitalini nchini Afrika Kusini mwezi Agosti baada ya kuugua ghafla akiwa kwenye ziara ya Rais Mugabe.
Hata hivyo, Mnangagwa mwenyewe alikanusha vikali tukio hilo kuhusishwa na Mama Grace.
Alisisitiza kuwa bado yeye ni mtiifu kwa Rais Mugabe na kwamba tuhuma dhidi ya Mama Grace kuhusu afya yake zinapaswa kupuuzwa.