Baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza mchakato wa uchaguzi wa udiwani kwa kata 43, mvutano umeanza tena ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kina kambi mbili hasimu.

Mvutano huo unatokana na namna ambavyo timu hizo za chama kimoja zinavyojipanga kuingia katika uchaguzi huo huku zikitofautiana mbinu na uamuzi wa kushirikiana au kutoshirikiana na kambi ya upinzani ya Ukawa.

Naibu Katibu Mkuu wa CUF upande wa Bara, Magdalena Sakaya ambaye anamuunga mkono Mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa timu hiyo ilifanya vikao juzi hadi usiku wa manane wakijadili jinsi ya kushinda uchaguzi huo.

“Miongoni mwa mambo ambayo tulijadili ni pamoja na kupitia kata moja baada ya nyingine kujua nguvu iko wapi ili tuweze kushiriki kwa asilimia 100,” Sakaya anakaririwa na Mwananchi.

“Tuliwasiliana pia na viongozi wa Wilaya ili kujua uhai wa chama wakati tunaelekea katika uchaguzi huu wa marudio,” alisema Sakaya na kuongeza kuwa hawatashirikiana na Ukawa katika uchaguzi huo.

Kwa upande wa kambi inayomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad imesema kuwa itashirikiana na Ukawa ili kuweza kuachiana kata.

“Kesho (leo) tutatoa taarifa rasmi. Lakini nasikia upande wa Profesa Lipumba hawataki ushirikiano. Nawaambia hawatashinda hata kata moja wakisimama peke yao,” alisema Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma wa CUF, Salim Bimani.

Ukawa inaundwa na vyama vya upinzani vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD. Vyama vyote vinapanga kuachiana kata huku CUF kukiwa na mvutano.

Uchaguzi huo unafanyika Novemba 26 mwaka huu ambapo msemaji wa CCM, Humphrey Polepole amesema kuwa hawana maneno mengi kwani kazi kubwa iliyofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano itajidhihirisha baada ya matokeo.

Polisi mbaroni kwa kumnyanyasa kingono mtoto wa kike akiwa selo
Mke wa Mugabe ashtukia mpango wa kumpindua Mumewe