Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack ameagiza halmashauri zote za mkoa huo kuhakikisha wanajumuisha bajeti ya kununua taulo za kike (sanitary pads) kwenye bajeti zao za mwaka ili kuwahudumia wanafunzi wa kike wa sekondari mkoani humo.
Hatua hiyo imeifanya Shinyanga kuwa mkoa wa mfano na wa kwanza kuchukua hatua kubwa zaidi za vitendo katika kuhakikisha wanafunzi wa kike wanahudhuria masomo yao wakiwa katika hali nzuri wawapo kwenye siku zao (hedhi).
Bi. Telack ambaye alitangaza hatua hiyo alipokuwa akizindua tamasha la jinsia katika wilaya ya Kishapu mkoani humo, alisema kuwa wanafunzi wa kike wanapaswa kusaidiwa kumaliza kwa mafanikio masomo yao na kwamba wanaume wanaowalaghai kuwapa mimba wanapaswa kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Mimi nadhani tuna tatizo sehemu. Kwasababu sheria iko wazi kwamba mwanaume anayempa mimba mwanafunzi wa kike anapaswa kufungwa jela miaka 30. Na kwa wale ambao wanabaka watakabiliwa na kifungo cha maisha jela. Lakini… Je, hii inatokea kwenye jamii yetu?” Alihoji.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa aliwaalika wadau mbalimbali wa elimu yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi, kuchangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wa kike kama sehemu ya hatua ya kuwalinda dhidi ya mazingira hatarishi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi aliyehudhuria tamasha hilo, aliipongeza halmashauri ya Kishapu, kwani mwaka jana iliweza kutenga fedha kwa ajili ya kugharamia taulo za kike kwa wanafunzi wa wilaya hiyo.