Mkutano wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) unatarajiwa kufanyika hapa nchini kuanzia tarehe 11 hadi 17 Machi, 2020 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushiriikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi amesema kuwa mkutano huo utafanyika kuanzia tarehe 12 hadi 17 Machi 2020 ambapo utatanguliwa na mkutano wa wataalamu pamoja na Makatibu Wakuu na kufuatiwa na mkutano wa mawaziri tarehe 16 – 17 Machi, 2020.
“Pamoja na mambo mengine, mkutano huu utahusisha Mawaziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mawaziri wa Fedha, Uchumi na Mipango pamoja na Mawaziri wa Viwanda na Biashara,” Amesema Prof. Kabudi
Waziri Kabudi amesema kuwa mkutano huo utahudhuriwa na Mawaziri 16 kutoka Nchi wanachama wa SADC za Angola, Namibia, Zambia, Zimbabwe, Comoro, Lesotho, Mauritius, Madagascar, Kongo DRC, Shelisheli, Msumbiji, Afrika Kusini, Tanzania, Malawi, Botswana pamoja na Eswatini)
Aidha, Kwa mujibu wa Mhe. Waziri Kabudi, Mkutano huo utakuwa mkutano wa kwanzawa SADC wa Baraza la Mawaziri kuendeshwa kwa lugha ya Kiswahili baada ya lugha hiyo kuwa miongoni mwa lugha rasmi za Jumuiya hiyo.
Prof. Kabudi aliongeza kuwa, mkutano huo utajadili masuala mbalimbali muhimu kwa mustakabali wa maendeleo na ustawi wa nchi wananchama wa SADC.
“Mkutano huu utapokea taarifa na kutolea maelekezo taarifa za vikao mbalimbali vya kisekta vya kamati za mawaziri ambavyo vimefanyika nchini tangu Septemba 2019,” Ameongeza Prof. Kabudi.