Kocha Msaidizi wa kikosi cha Young Africans, Charles Boniface Mkwasa, amesema wachezaji wa klabu hiyo wanapaswa kuendelea na mazoezi binafsi bila kuchoka, wakati wakisubiri hali ya janga la Corona kumalizika na kocha wao mkuu, Luc Eymael, kurejea nchini kutoka Ubelgiji.
Eymael amekwama kwao kutokana na janga la virusi vya Corona lililosababisha safari za ndege za kimataifa kuzuiwa hadi hali itakapokuwa nzuri.
Mkwasa aliyekuwa kocha wa muda klabuni hapo baada ya Mwinyi Zahera kutimuliwa, pia amewataka wachezaji kuepuka kupata virusi vya Corona, huku akiwasisitiza kutosahau programu walizopewa kila mmoja kwa kujiimarisha kwa mazoezi.
“Wachezaji waendelee na mazoezi huku wakijilinda na virusi vya Corona, naamini muda sio mrefu kocha atarejea na kutoa maelekezo mengine, wasichoke wapambane kujenga mwili kimazoezi, ” alisema Mkwasa.
Baadhi ya wachezaji wa Young Africans wameonekana kuitikia wito wa kufanya mazoezi wakiwa nyumbani kwa muda mrefu sasa.
Hadi ligi inasimama, Young Africans ilikuwa katika nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 51, nyuma ya Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa alama 54 huku mabingwa watetezi Simba SC wakishikilia usukani kwa kumiliki alama 71.