Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), inawashikilia watuhumiwa 11 akiwemo Mmiliki wa Kituo cha Cambiasso Sports Academy, Kambi Zubeir Seif (40), na Kocha wa Makipa wa Timu Simba Sports Club, Muharami Said Sultan (40), baada ya kukamata kilo 34.89 za Dawa za kulevya aina ya Heroin na Biscuit 50 zilizotengenezwa kwa kutumia Bangi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Gerald Kusaya iliyotolewa hii leo Novemba 15, 2022 imeeleza kuwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao kumefanikishwa kwa ushirikiano na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, baada ya operesheni mbalimbali nchini.
Amewataja watuhumiwa wengine kuwa ni Said Abeid Matwiko (41), Maulid Mohamed Mzungu (54), John Andrew Chipanda (40), Rajabu Mohamed Dhahabu (32), Seleman Matola Said (24), Hussein Mohamed Pazi (41) na Ramadhan Rashid Chalamila (27), ambao wote kwa pamoja wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani.
Katika tukio la pili, DCEA imemkamata mfanyabiashara, Abdulnasir Haroun Kombo (30), akiwa na biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi, kama malighafi aliyokuwa anaiuza maeneo ya Kaloleni jijini Arusha akiwa na mtuhumiwa mwingine Hassan Ismail (25), ambaye anasadikika kuwa ndiye mtengenezaji wa bidhaa hiyo.
Kufuatia matukio hayo, DCEA imewakumbusha wananchi kuwa, kujihusisha kwa namna yeyote na dawa za kulevya ni kosa kwa mujibu wa sheria ya kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya sura ya 95 ambayo inatoa adhabu ya kifungo cha maisha huku ikiwataka kushiriki kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya.
Matukio ya uwepo wa bidhaa za vyakula vinavyotengenezwa kwa kutumia bangi yamemekuwa yakiripotiwa nchini ambapo mwaka 2020 na 2021 Mamlaka hiyo ilikamata bangi iliyosindikwa mfano wa jam, keki na asali katika maeneo tofauti wakati DCEA ikitekeleza majukumu yake huku ikiwaomba wananchi kuwa makini na ununuzi wa bidhaa bila umakini.