Sekretarieti ya Shirikisho la Soka Tanzania ‘TFF’ imemfungulia Mashatka mbele ya Kamati ya Maadili Kocha Mkuu wa Kikosi cha Vijana cha Azam FC chini ya umri wa miaka 17 Mohamed Badru.
TFF imethibitisha kufungua Mashataka hayo kupitia taarifa maalum iliyosambazwa katika Mitandao ya Kijamii, ikieleza dhamira ya kufanya hivyo dhidi ya Kocha Badru.
Badru anadaiwa kuwasilisha vyeti visivyo sahihi, hivyo hakuwa na sifa ya ukufunzi wa Soka katika klabu alizozifundisha na timu ya vijana ya Azam FC chini ya Umri wa miaka 17.
Badru amewahi kuzinoa klabu za Gwambina FC na Mtibwa Sugar zikiwa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kamati ya Maadili ya TFF kupitia kwa Mwenyekiti wake tayari imepewa taarifa kuhusu malalamiko dhidi ya Badru, hivyo itapanga siku ya kusikiliza shauri hilo, na Mlalamikiwa atapewa taarifa.
Kocha Badru jana Jumapili (Julai 24) alikiwezesha kikosi cha Vijana chini ya Umri wa miaka 17 cha Azam FC kutwaa Ubingwa wa Ligi ya Vijana wa umri huo kwa kuifunga Pan Africans mabao matano.