Sakata la Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi limeendelea kuzua matamshi na mitazamo mbalimbali ambapo leo, Mbunge wa Siha, Dkt. Godwin Mollel (CCM) amesema kuwa ulikuwa mpango wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Dkt. Mollel ambaye alikuwa mbunge wa Chadema na baadaye kuhamia CCM ambako aligombea tena na kurejea bungeni akiwa amebadili chama, ameliambia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa yeye aliiba sampuli ambazo chama hicho kilimkataza kuzitumia.

Mbunge huyo amedai kuwa alipojaribu kuwasilisha sampuli hizo ili zipelekwe Afrika Kusini kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi alikataliwa na uongozi wa chama hicho kikuu cha upinzani kwa kile alichodai walifahamu kuwa wangeumbuka.

“Mimi nilikuwa huko lakini nilikimbia kwa mipango yao, hata katika tukio la kushambuliwa Lissu mimi niliingia ndani kwenye uchunguzi na niliiba baadhi ya vitu lakini walikataa mapendekezo yangu,” alisema Mollel.

Hata hivyo, wabunge wa Chadema, Frank Mwakajoka (Tunduma) na Joseph Selasini (Rombo), kwa nyakati tofauti waliomba kutoa taarifa kuhusu hoja ya Mollel ambapo walimtaka mbunge huyo kuthibitisha kauli zake na kutovunja kiapo chake cha udaktari.

Akijibu kuhusu taarifa hiyo, Dkt. Mollel alidai kuwa ili athibitishe anataka Chadema waeleze wanakopeleka ruzuku za chama hicho pamoja na kile alichodai kuwa ni mpango wao dhidi ya Zitto Kabwe na marehemu Chacha Wangwe walipojaribu kugombea uenyekiti wa chama hicho.

Lissu amekuwa mjadala kwa nyakati tofauti ndani ya Bunge wiki hii kutokana na kauli anazozitoa hivi karibuni katika ziara zake za ughaibuni. Spika wa Bunge ameahidi kufanyia kazi hoja iliyowasilishwa na Mbunge wa Geita, Joseph ‘Msukuma’ Kasheku kuwa ofisi ya Bunge isitishe mshahara na stahiki za Lissu.

Mbunge huyo wa Singida Mashariki jana aliiambia Sauti ya Amerika kuwa anaendelea na matibabu na anatarajia kufanyiwa upasuaji wa 23 nchini Ubelgiji.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Februari 9, 2019
Chadema wamshtaki Wallace Karia, 'Haiwezekani atoe kauli ya kichochezi'