Kufuatia Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kumuondoa mwanawe, Muhoozi Kainerugaba, kama kamanda wa majeshi ya nchi kavu ya Uganda, baada ya kutishia kwenye Twitter kuivamia nchi jirani ya Kenya na kumpa cheo cha juu Jeshini na kuwa Jenerali kamili na kubakia na wadhifa wake kama mshauri wa rais katika shughuli maalum, baadhi ya wananchi wameibuka na maoni tofauti.
Kainerugaba, anayejulikana kama mkuu wa jeshi na mrithi aliyechaguliwa na babayake, baadaye alisema maoni hayo aliyoyatoa Octoba 3, 2022 yalikuwa ni ya mzaha, kitu ambacho kinapingwa na baadhi ya watu hasa wanadiplomasia wanaodai kitendo hicho si kizuri kwani kinahatarisha mahusiano.
Kwa nyakati tofauti, Wananchi hao wakiwemo wanadilpomasia wamedai Kainerugaba anazungumza waziwazi kwenye mitandao ya kijamii, mara kwa mara, akifanya biashara ya vijembe kwa viongozi wa upinzani na kujikita katika siasa, ingawa jukumu lake la kijeshi linamzuia kufanya hivyo na wanasema kiburi hicho anakipata kwa baba yake (Rais Museveni).
Jumatatu na Jumanne (Oktoba 3 – 4, 2022), Muhoozi alituhumiwa kuchapisha jumbe za uchochezi kwenye Twitter, zikiwemo za kupendekeza kuunganishwa kwa Kenya na Uganda, kuivamia Kenya na kuiteka Nairobi ndani ya siku 14, kuangusha utawala wa Ruto na kutoa ng’ombe 100 ili kumuoa Kiongozi anayetarajiwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Italia, Giorgia Meloni.
Maoni yake hayo, yalivutia hasira za umma kutoka kwa Wakenya kwenye mitandao ya kijamii, ambapo Wizara ya mambo ya nje ya Uganda katika taarifa yake hapo jana (Oktoba 5, 2022) iliahidi “kuishi pamoja na kwa amani” na nchi jirani ya Kenya lakini ikashindwa kurejelea ujumbe wa Twitter wa Kainerugaba.
Hata hivyo, katika kile kinachoonekana ukosefu wa maadili, mara baada ya jeshi kutoa tamko lake la kupandishwa cheo kwa mtoto huyo wa Museveni, Kainerugaba alichapisha tena jumbe za kujipongeza na kusema sasa anafaa kugombea urais katika uchaguzi ujao na kwamba “Tunaenda kufanya sherehe chini ya Barabara ya Kampala, namshukuru baba yangu kwa heshima hii kubwa!”
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Uganda, na baadhi ya viongozi wa upinzani kwa muda mrefu wamekuwa wakimshutumu Rais Museveni (78), kwa kumlea mwanawe ili achukue hatamu kutoka kwake, lakini Museveni ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 36 amekuwa akikana kufanya hivyo mara kwa mara.